Makala yaliyopendekezwa ya Jarida la Kiarabu la Kimataifa, mwezi Sept idadi ya maneno 699.
Muungano wa Ulinzi: Je, inawezekana kuunda jeshi la pamoja la Kiafrika au Kiarabu?
Na: Rami Zuhdi, Mtaalamu wa Masuala ya Kisiasa na Kiuchumi ya Afrika
Kwa miongo kadhaa, ndoto ya kuwa na umoja wa kijeshi imekuwa ikijitokeza mara kwa mara katika hotuba za kisiasa katika ulimwengu wa Kiarabu na wa Kiafrika. Mitazamo inatofautiana kati ya wale wanaoiona kama hitaji la kimkakati mbele ya vitisho vinavyoongezeka, na wale wanaoiona kama ndoto isiyowezekana kutokana na changamoto za uhuru wa kitaifa, migongano ya maslahi, na tofauti za kijiografia na kisiasa. Kati ya ndoto na uhalisia, maswali ya kistratejia yanabaki: Je, kweli inawezekana kuunda jeshi moja la pamoja, au angalau mfumo wa ulinzi wa pamoja unaofanya kazi katika nyanja za Kiarabu na Kiafrika?
Katika mazingira ya sasa na vitisho vinavyofanana, bara la Afrika na ukanda wa Kiarabu unakabiliwa na changamoto zinazoshabihiana. Kuna ugaidi unaovuka mipaka katika eneo la Sahel na Jangwa la Sahara, Bonde la Ziwa Chad na Pembe ya Afrika. Pia vitisho vinavyoendelea kutoka kwa makundi ya Daesh na Al-Qaida kaskazini mwa Afrika, pamoja na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan, Libya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambavyo vimeunda mazingira dhaifu yanayowaruhusu wageni kuingilia kati. Aidha, usalama wa maji na chakula nao ni masuala ya kimkakati yasiyopaswa kupuuzwa kwa kuwa ni hatari kama hatari zile za kijeshi.

Vilevile, kuna uwepo mkubwa wa kijeshi wa kigeni barani Afrika (zaidi ya kambi 13 za Marekani, kambi 5 za Ufaransa, pamoja na uwepo wa Urusi, Uturuki, Iran na China), hali inayoonyesha ukubwa wa ushindani wa kimataifa barani humo.
Janga kubwa zaidi ni mashambulizi ya mara kwa mara ya Israel dhidi ya nchi za ukanda huu kama Syria, Iraq, Lebanon, Yemen na hivi karibuni Qatar. Haya yote yanakuja sambamba na mauaji ya kikabila na uhalifu wa kivita dhidi ya wananchi wa Palestina, iwe Gaza au Ukingo wa Magharibi. Hali hii inalazimisha kutafuta mbinu ya pamoja badala ya suluhisho za kila nchi pekee ambazo zimethibitika kuwa na udhaifu mkubwa.
Mfano wa Umoja wa Ulaya na NATO unafaa kuzingatiwa. Japokuwa Ulaya imeunganishwa kiuchumi, haikuweza kuunda jeshi moja la pamoja, bali iliunda mifumo ya ulinzi inayoshirikiana chini ya mwamvuli wa NATO. Huu ni mfano wenye thamani ya kutafakariwa.
Barani Afrika, iliundwa African Standby Force (ASF) mnamo 2003, ikikusudiwa kuwa na majeshi ya kikanda 5 yenye askari wapatao 25,000. Hata hivyo, hadi leo bado imebaki kuwa mradi uliokwama kutokana na matatizo ya kifedha na udhaifu wa nia ya kisiasa.
Aidha, muungano wa Kiarabu nchini Yemen ulikuwa ni uzoefu wa vitendo ulioonesha uwezo wa uratibu wa kijeshi kati ya majeshi ya Kiarabu, lakini pia ulidhihirisha changamoto za tofauti za kistratejia na uwezo wa kijeshi.
Hili si jambo rahisi. Kwa mfano, suala la uhuru wa kitaifa bado ndilo kikwazo kikubwa zaidi, kwani mataifa hayako tayari kukabidhi mamlaka ya kijeshi kwa chombo cha pamoja.
Pia kuna pengo kubwa la matumizi ya kijeshi: Algeria na Misri peke yao hutumia zaidi ya dola bilioni 20 kwa mwaka, ilhali nchi nyingi za Kiafrika kwa pamoja hazifiki hata dola milioni 500 kila moja.
Kuna pia tofauti za kiwango cha maandalizi ya kijeshi. Jeshi la Misri ni miongoni mwa makubwa zaidi katika eneo (zaidi ya askari 450,000, na zaidi ya askari 800,000 wa akiba), likifikia jumla ya karibu askari milioni 1.4, wakati baadhi ya majeshi mengine hayazidi askari 10,000.
Aidha, miundombinu ya ulinzi ni changamoto. Kukosekana kwa viwanda vya kijeshi vya ndani katika nchi nyingi kunazifanya kutegemea uagizaji kutoka nje, jambo linalodhoofisha uwezo wa kujitegemea katika ulinzi.
Kwa hiyo, wazo la jeshi moja kubwa la pamoja linabaki kuwa ndoto nzuri lakini isiyowezekana katika muda mfupi, kutokana na changamoto za uhuru na tofauti za kiuchumi. Huenda suluhu ya vitendo zaidi ikawa uundaji wa vikosi vya kikanda vya pamoja, kama vile nguvu ya Kiarabu katika Bahari Nyekundu na Ghuba ya Aden kwa ajili ya kupambana na uharamia na ugaidi wa baharini, au nguvu ya Kiafrika katika eneo la Sahel na Sahara.
Vivyo hivyo, kuanzishwa kwa vituo vya pamoja vya uongozi vinaweza kusaidia kukuza mifumo ya uongozi wa kijeshi ya kikanda kwa madhumuni ya uratibu wa mafunzo, ujasusi na mazoezi ya kijeshi.
Pia, kuna haja ya ushirikiano wa viwanda vya kijeshi, kwa kuimarisha ushirikiano katika sekta ya ulinzi, mfano wa ushirikiano wa Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu, au Misri na Afrika Kusini, ili kujenga msingi wa ndani wa uzalishaji wa silaha utakaoisaidia miungano ya ulinzi.
Misri, kwa nafasi yake ya kijiografia na uzito wake wa kijeshi na kisiasa, ina uwezo wa kuchukua uongozi katika kuunda mfumo wa ulinzi wa Kiarabu-Kiafrika, kupitia kuanzisha vituo vya mafunzo vya pamoja vya kikanda, kuimarisha viwanda vya kijeshi vya pamoja kwa kushirikiana na mataifa ya Kiarabu na Kiafrika, na pia kusukuma Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kufufua mikataba ya ulinzi wa pamoja iliyositishwa kwa miongo mingi.
Kwa hakika, muungano wa ulinzi si anasa, bali ni hitaji la kimsingi katika dunia inayobadilika kwa kasi, ambapo vitisho vya kiusalama havibaki vya kijeshi tu, bali pia vinahusu usalama wa kimtandao, maji na uchumi. Kuunda jeshi moja la pamoja huenda likawa mbali, lakini kujenga mitandao ya kikanda ya ulinzi inayoshirikiana kikamilifu ndilo chaguo la kivitendo zaidi kwa sasa, na hatua ya taratibu kuelekea ulinzi wa pamoja kwa siku zijazo.
Ni jukumu la kisiasa na kihistoria linalobebwa na watoa maamuzi barani Afrika na katika ulimwengu wa Kiarabu, kutambua kwamba usalama hauwezi kugawanywa, na kwamba mustakabali utalindwa tu na nguvu ya pamoja yenye busara, inayoanzia katika mshikamano na siyo ushindani.


