Nchini Sudan: “Ni ndoto za mchana kweupe – Wanamgambo wa RSF kutangaza Serikali isiyo na nchi Wala Uhalali”
“Serikali bila ya nchi... Mamlaka isiyo na Uhalali: Uchambuzi wa Kistratejia kuhusu Tangazo la Wanamgambo wa RSF Kuunda Serikali yao nchini Sudan

Na Rami Zuhdi – Mtaalamu wa Masuala ya Afrika
Kati ya bunduki inayohema kwa hofu na bendera bandia isiyo na nguvu, ndipo “serikali ” ya Hemeti (Mohamed Hamdan Dagalo) ilipozaliwa. Ilizaliwa ikiwa imeharibika, tasa, na haina matumaini ya kuishi hata kwa siku chache – hata kama ingewahi kupata “huduma ya dharura ya kisiasa” kuokoa kizazi hicho cha kisiasa kilichozaliwa kikiwa kinaugua. Ni mamlaka ya majivu tu, serikali isiyo na wananchi, isiyo na nchi, na isiyo na mustakabali. Ni nani atakayeamini udanganyifu wa Hemeti, anapojitangaza kuwa na serikali ambayo haina chochote zaidi ya ndoto za kushindwa zilizoahirishwa bila ya nchi.
Katika wakati ambapo vurugu inachanganyika na upuuzi, na uharibifu unashirikiana na propaganda, kiongozi wa RSF – Mohamed Hamdan Dagalo maarufu kama “Hemeti” – alitangaza kuunda kile alichokiita “Serikali ya Kiraia ya Sudan” katika maeneo anayodai kuyadhibiti huko Darfur. Hatua hii, kidhahiri ni “ujasiri wa kisiasa”, lakini kimsingi haikuwa chochote zaidi ya kielelezo cha kuporomoka kwa maadili ya kisiasa na kijeshi, na ni kielelezo cha kushindwa kwake, ambacho hakina budi kuja, baada ya zaidi ya miaka miwili ya kuwasha moto wa vita, na kuivuta Sudan kutoka kwenye demokrasia hadi kwenye giza la mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, mgawanyiko na kusambaratika.

Swali kuu ni: Tangazo la serikali hii isiyo na nchi, isiyo na utambuzi wa kikanda wala wa kimataifa, na isiyo na msingi wowote wa kisheria au kiserikali, linamaanisha nini? Tunapaswa kuliona kama nini katika mazingira haya? Na ni madhara gani ya kisiasa na kiusalama yanayoweza kuikumba Sudan, kanda ya Afrika Mashariki na Kati, na bara lote? Je, tunashuhudia jaribio lengine jipya la “kujenga fikra ya kujitenga kwa upole” (soft secession) au ni jitihada ya kukata tamaa ya kudumisha sura ya mamlaka iliyokwishadhoofika, kupitia “serikali ya kivuli” isiyoweza kudumu mbele ya uchambuzi wa kistratejia.
Ni muhimu kubaini kuwa tangazo la Hemeti mnamo Julai 2025 lilikuja katika kipindi ambacho RSF ilikuwa inakumbwa na kuporomoka kwa nguvu zake za kijeshi na kisiasa, hasa baada ya kupoteza udhibiti katika ngome kadhaa muhimu za Darfur Magharibi, pamoja na kufichuliwa kwa ukatili wake dhidi ya raia katika miji ya El Geneina na Nyala – kwa mujibu wa ripoti rasmi za mashirika ya kimataifa. Hivyo basi, tangazo hili halikuwa zaidi ya mbinu ya propaganda, lililolenga kujipatia nafasi mpya ya kisiasa baada ya kushindwa kimapigano, na jaribio la kuunda kadi mpya ya majadiliano kwa kuonyesha picha ya “serikali ya kiraia mbadala”, ikionekana kana kwamba kuna upande halali wa kisiasa unaoweza kuzungumza nao, sambamba na serikali rasmi iliyo mjini Port Sudan.
Lakini hali halisi ni kwamba “serikali” hiyo si zaidi ya mamlaka ya kufikirika, imefungiwa katika upweke wa kisiasa na imeegemea kwenye ardhi yenye migongano ya kijeshi. Kisheria na kikatiba, RSF haina uhalali wowote wa kuunda serikali: Ni kundi la wanamgambo lisilo chaguliwa, linashiriki katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, na sehemu kubwa ya wapiganaji wake ni mamluki kutoka mataifa mengine. Ni kundi lililoshutumiwa kwa uhalifu wa kivita dhidi ya raia (kama ilivyoripotiwa na Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Human Rights Watch, Amnesty International na mashirika mengine ya usalama na siasa).
Kwa hivyo, tangazo lao la kuunda serikali halina nguvu ya kisheria, bali ni sehemu ya vita vya habari na propaganda – na si tukio la kimsingi lenye athari ya kweli ya kisiasa. Kistratejia, jambo hili linapaswa kueleweka kwa kuzingatia malengo yake: Ni kwa ajili ya matumizi ya ndani zaidi, likielekezwa kwa wafuasi wachache wa RSF, ili kuendeleza taswira ya “dola” kichwani mwao, wakati hamasa ya mapigano ikianza kudhoofika na hasara zikionekana wazi.
Pia, ni ujumbe wa mazungumzo kwa jamii ya kimataifa – RSF (Rapid Support Forces) inajaribu kuuza taswira bandia kwamba ina sura ya kiraia inayoweza kuifanya ishirikishwe kisiasa, katika juhudi zisizo na mafanikio za kufufua wazo la kugawana madaraka. Lakini uhalisia wa kisiasa, kisheria na wa kijeshi hauna ushahidi wowote wa kuiunga mkono.
Aidha, kuna matumaini ya kudumu kutoka kwa baadhi ya wahusika wa kimataifa wanaotafuta kufufua ndoto ya “kujiondoa kwa upole” (soft secession) nchini Sudan tangu siku za kwanza za vita – ndoto ambayo huenda ndiyo sababu vita hivyo vilianzishwa, vikapangwa na kuendeshwa kutoka nje. Katika mtazamo huu, tangazo la Hemeti linaweza kuonekana kama hatua ya kimbinu kuelekea kujitenga kwa Darfur, au angalau kuunda mamlaka ya ukweli wa muda (de facto) magharibi mwa Sudan. Hata hivyo, ni hali inayotishia mustakabali wa Sudan kama dola moja yenye umoja wa kijiografia na kisiasa.
Athari za tangazo hili katika mgogoro wa Sudan ni nyingi, lakini zenye uzito mdogo.
Kijeshi na kimaeneo: hakuna athari halisi; Tangazo la RSF halijatafsirika kuwa miundo ya serikali inayoonekana. Hakuna wizara, hakuna taasisi za utawala, hakuna mifumo ya utoaji huduma. Ni majina tu na vyeo hewa visivyo na muundo wa utendaji – katika maeneo ambayo tayari yanakumbwa na janga la wakimbizi wa ndani na nje zaidi ya watu milioni 8, kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa (2025).
Kisiasa: ni jaribio la kuleta ushaiwshi tu, bila kubadilisha mizani ya nguvu wala mwelekeo wa mataifa, ambayo yote yanatambua serikali rasmi ya Sudan na Baraza la Uongozi linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, kama mamlaka halali kwa mujibu wa utambuzi wa kikanda na kimataifa.
Ni jambo la kawaida na la lazima mataifa kuunga mkono taasisi rasmi za Sudan na jeshi lake la kitaifa, kwa kuwa kuunga mkono wanamgambo wa kujitenga dhidi ya wananchi na dola yoyote ni uhalifu wa kivita na kitendo cha uhasama wa kisiasa.
Kikanda, tangazo hili linaongeza hatari, kwani linaweka mfano mbaya unaoweza kuhamasisha makundi mengine ya waasi kuiga mbinu hiyo – na kusababisha mlipuko wa “serikali kama hizi” barani Afrika ikiwa halitashughulikiwa kwa uthabiti wa kisheria, kisiasa na kimaelezo. Hatari hii inahusu Sudan moja kwa moja, lakini pia nchi nyingine ndani na nje ya bara la Afrika.
Aidha, ujumbe wa kisiasa ni wazi: Hemeti si tena kiongozi mwenye nguvu uwanjani; sasa ni mchezaji aliyekata tamaa, anayeshika “karata zilizochomwa”. “Serikali” aliyoitangaza haina maana zaidi ya kuwa kioo cha propaganda cha genge la kijeshi, linalojaribu kuvaa sura ya uhalali, huku rekodi yake ya damu ikiendelea kulifukuza kila linapojaribu kujitokeza kimataifa.
Katika kamusi ya siasa za Kiafrika, tunafahamu kwamba uhalali haujengwi kwa matangazo, bali kwa taasisi, uungwaji mkono wa wananchi, utambuzi wa kimataifa na udhibiti wa nchi.
Hata hivyo, licha ya ujuu juu wa tangazo hili lisilo na uhalali, kuna haja ya hatua thabiti dhidi yake:
1. Harakati ya kidiplomasia ya dharura ya Misri–Afrika: Cairo, ikiwa mwenyeji wa mchakato wa kisiasa wa Sudan ndani ya Umoja wa Afrika, inapaswa kuchukua jukumu la kuunga mkono serikali halali na kupinga kwa nguvu zote jaribio lolote la kuigawanya Sudan. Hii ni kwa sababu Misri ndiyo jirani iliyo karibu zaidi, yenye ushawishi mkubwa na yenye uhusiano wa kihistoria na watu wa Sudan – na pia ndiyo nchi inayoguswa moja kwa moja na madhara ya mgogoro wa Sudan.
2. Ushirikiano wa kikanda: Kushirikisha mataifa jirani (Chad, Libya, Sudan Kusini, Ethiopia, Eritrea) kuhakikisha hakuna utambuzi au ushirikiano na kiumbe hiki kisicho halali.
3. Kuimarisha mchakato wa mazungumzo ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika: Shinikizo la pamoja la kimataifa linafaa kurudisha meza ya mazungumzo kati ya serikali halali na makundi ya silaha, mbali na usanii wa “serikali hii”.
4. Mapambano ya habari: Ni lazima kufichua uongo unaoenezwa na RSF, kusajili ukiukaji wake na kuonyesha hadharani uhalifu wake – kama kipaumbele cha kidiplomasia na kisiasa, kwa kushirikiana na washirika wa kimataifa.
Mwisho wa yote, kile kinachoitwa “serikali” si zaidi ya udanganyifu uliofungwa ndani ya kushindwa. Ni jitihada ya kukata tamaa kushikilia mabaki yasiyo na thamani – sura ya uongo ya dola isiyokuwepo. Ni kivuli cha mamlaka iliyopotea, na propaganda ya genge linaloendelea kutenda uhalifu kwa jina la dola.
Kutokana na jukwaa hili, natoa wito kwa nguvu zote za Kiafrika na Kiarabu kuungana na Sudan, kuunga mkono umoja wake, na kukataa mipango yote ya kujitenga au juhudi za kufufua migogoro kwa kutumia nyuso za kisiasa za udanganyifu.
Kwa hakika, hatari haipo kwenye tangazo la “Hemeti” pekee, bali ipo katika kulipitisha kimyakimya au kulinyamazia.


